Tuesday, 17 September 2013

LICHA ya adha wanayoipata wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanaoishi shule maalumu ya Bughangija iliyopo manispaa ya Shinyanga ikiwemo uhaba wa chakula, matibabu pamoja na makazi bora lakini bado wazazi na walezi wa watoto hao hawana njia ya kulinda usalama wao zaidi ya kuendelea kuwapeleka shuleni hapo.

Watoto hawa (Pichani) wakiwa na wazazi wao wakiingia shuleni hapo juzi na kuongeza idadi ya wanafunzi waliopo shuleni hapo zaidi 100 waliolazimika kutengana na familia zao kutokana na kuibuka kwa wimbi la mauaji ya walemavu wa ngozi nchini hususani katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora.

Saturday, 7 September 2013

WANAFUNZI WABADILISHA CHUMA CHAKAVU KWA MADAFTARI

Ule usemi kwamba ukitaka elimu huna budi kuitafuta "popote na kwa gharama yoyote" umewaingia wanafunzi wa shule ya Msingi Mwampunga Bule iliyopo kata ya Mishepo wilaya ya Shinyanga vijijini waliolazimika kubadilishana vyuma chakavu na wafanyabiashara wa bidhaa hizo ili kupata mahitaji yao ya shule.

Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya wazazi kukosa mwamko wa elimu hivyo kuacha kuwahudumia watoto wao mahitaji yao ya shule ambapo biashara hiyo inawasaidia wanafunzi hao kupata mahitaji muhimu kama vile madaftari, kalamu pamoja na mabegi ya kubebea madaftari.

Njia hii imebuniwa na baadhi ya wanafunzi wanaopenda elimu, jambo ambalo pia limeungwa mkono na walimu wa shule hiyo baada ya kuona ni mkombozi kwa wanafunzi hao.

HAYA NDIYO MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA?

 
Hii ni shule ya Msingi Majahida iliyopo nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu ambapo nusu ya wanafunzi wake hukalia mawe madarasani kutokana na uhaba mkubwa wa madawati shuleni hapo.

Wilaya ya Bariadi inaongoza nchini kwa kuzalisha pamba asilimia 60, pia ina rasilimali ya madini pamoja na mifugo ya aina mbalimbali.